KITUO CHA UCHENJUAJI DHAHABU JEMA AFRIKA CHAPEWA ONYO LA MWISHO
Kahama,
Waziri wa Madini Doto Biteko ametoa Onyo la Mwisho la Kukifungia Kituo cha Uchenjuaji Dhahabu cha Jema Afrika kilichopo Wilayani Kahama.
Hatua hiyo inafuatia kubainika kwa jaribio la wizi wa dhahabu uliofanywa na baadhi ya wafanyakazi wa kituo hicho kutaka kuiba dhahabu ya mteja.
Akizungumzia tukio hilo, Waziri Biteko amewataka wamiliki wa kituo hicho kuandika barua ya kuweka makubaliano na Serikali ya kutojirudia tena kwa vitendo vya wizi kituoni hapo.
"Ni jicho la huruma tu tukiwapeleka mahakamani mali zenu zitataifishwa. Tunajua mmewekeza mitaji yenu na mna mikopo. Nilishamwambia mmiliki kuwa kituo chako kina rekodi ya wizi. Rais anawapenda, anawapigania ili watanzania wamiliki uchumi wa madini lakini mnamuangusha kwa kutofuata taratibu," amesisitiza Waziri Biteko.
Amewatahadharisha wamiliki wa vituo vya uchenjuaji nchini kuhusu wizi wote wa dhahabu unaofanyika na kuwasisitiza kwamba, unafahamika na kuwataka wote wanaojihusisha na vitendo hivyo kujiepusha na kwa wale wasiotaka kufanya kazi zao kwa uaminifu watafute biashara nyingine.
Mbali na kutembelea kituo hicho, pia, Waziri Biteko na ujumbe wake wametembelea Kituo Kidogo cha Ununuzi wa dhahabu kilichopo katika eneo la Wachimbaji wadogo wa Mwime ambapo amewapongeza kwa kufuata taratibu na Sheria na kuwataka kufanya kazi zao kwa amani.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Zainab Taleck amesema Mkoa huo unahitaji wawekezaji lakini walio waaminifu.
Ameongeza kuwa, wizi na udanganyifu katika kiwanda cha uchenjuaji Jema Africa ulibainiwa na Kamati ya Ulinzi na Usalama na kutumia fursa hiyo kuwatahadharisha wote wasiofuata taratibu kuwa serikali inawaona na itawafikia.
Katika ziara hiyo, Waziri Biteko pia ameongozana na Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo , Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Shinyanga, Kamishna wa Madini Mhandisi David Mulabwa na Watalaam kutoka Tume ya Madini.
Aidha, ziara hiyo imefanywa wakati ambapo wizara na wadau wengine wa madini wanashiriki Maonesho ya Pili ya Teknolojia na Uwekezaji kwenye Sekta ya Madini Mkoani Geita yanayotarajiwa kuhitimishwa Septemba 29, 2019.
TEITI Office Dodoma
Postal Address: S.L.P 361 Kikuyu Ave.
Telephone: +255688386546
Mobile: +255688386546
Email: info@teiti.go.tz
Haki Miliki ©2017 TEITI .Haki zote Zimehifandiwa