Ripoti 12 za TEITI zabainisha Serikali Yakusanya Dola za Marekani Bilioni 4.30
Yasisitizwa kuanzisha Mfumo utakaowezesha kukusanya takwimu za Wachimbaji Wadogo
Wananchi waelezwa wanayo haki ya kupata taarifa ya namna kampuni zinavyochangia
Asteria Muhozya na Godwin Masabala - Mirerani
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Madini Msafiri Mbibo amesema kwamba, ripoti 12 zenye takwimu za malipo ya kampuni za madini na gesi asilia zilizowekwa wazi na Taasisi ya Uhamasishaji Uwazi na Uwajibikaji katika Rasilimali za Madini, Mafuta na Gesi Asilia (TEITI), kwa kipindi cha Julai 2008 hadi Juni 30, 2020 zimebainisha kuwa, Serikali imekusanya kiasi cha dola za Marekani bilioni 4.30.
Ameyasema hayo wakati akifungua warsha ya kuelimisha Madiwani, Asasi za Kiraia, Viongozi wa Halmashauri na Wachimbaji Wadogo kuhusu matumizi ya takwimu zinazotolewa na taasisi hiyo iliyofanyika Desemba 7, 2022, katika Mji Mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoa wa Manyara.
Ameongeza kwamba, uchambuzi wa ripoti za TEITI utawasaidia wananchi kufahamu kwa uwazi na uhakika aina na kiasi cha kodi au tozo zinazolipwa na kampuni serikalini, gharama za uwekezaji na uzalishaji katika sekta za madini, gesi na mchango wa uwekezaji mkubwa katika uchumi wa Taifa.
‘’Takwimu hizo zikiwa wazi zinasadia wananchi kutambua fursa zilizopo katika kushiriki masuala ya kiuchumi na vilevile kufahamu michango na wajibu wa kampuni kwa jamii’’ amesema Mbibo.
Ameeleza kwamba, kufuatia umuhimu wa ripoti hizo na kwa kuzingatia dhamira ya Serikali kuendesha shughuli zake kwa uwazi, na kwa kutambua kwamba si wadau wote wanaoweza kuchambua takwimu na taarifa zinazopatikana katika ripoti za TEITI, Serikali imeona upo umuhimu wa kuwajengea uwezo wadau hao kuhusu namna ya kuchambua takwimu hizi pamoja na kuzitumia katika kuhoji na kuibua mijadala itakayosaidia kuboresha sekta hii ya uziduaji.
‘’Ripoti za TEITI ni nyaraka na nyenzo muhimu sana. Ripoti hizi zinaweka wazi takwimu mbalimbali za malipo ya kodi na tozo nyingine zinazolipwa serikalini na kampuni za madini, mafuta na gesi asilia. Ripoti hizi zikiwafikia wananchi kwa wakati zitasaidia kutoa majibu ya maswali ya wananchi juu ya mchango wa sekta za madini, mafuta na gesi asilia katika uchumi wa nchi yetu” amesisitiza.
Katika hatua nyingine, ameisisitiza TEITI kufanyia kazi maelekezo ya Waziri wa Madini Dkt. Doto Biteko kuhusu kuanzisha mfumo mzuri utakaowezesha urahisi wa kukusanya takwimu za malipo yanayofanywa na wachimbaji wadogo wa madini kwa Serikali.
‘’Hii itarahisisha uwekaji wazi wa takwimu hizo na kuweka kumbukumbu sahihi juu ya mchango wa wachimbaji wadogo katika mapato ya Serikali. Ninawasihi wawakilishi wa vyama vya wachimbaji wadogo mliopo hapa mkawe mabalozi wazuri wa TEITI kwa kuelimisha wachimbaji wengine juu ya takwimu za TEITI na muipatie TEITI ushirikiano wa kutosha ili kufanikisha uwekaji wazi wa takwimu kutoka katika shughuli zenu za uchimbaji,’’ amesema.
Pia, amewataka wadau hao kutambua kuwa, masuala ya kutoa huduma na bidhaa katika migodi na uwajibikaji wa Kampuni kwa Jamii yapo kisheria na ni jukumu la kila kampuni kuweka mipango madhubuti ya namna ya kusaidia kuyatekeleza na kueleza kuwa, ‘’ ninatambua kuwa ripoti za TEITI zinahusisha takwimu kuhusu ushiriki wa watanzania katika kutoa huduma na bidhaa katika migodi (Local Content) na Uwajibikaji wa Kampuni kwa Jamii (CSR)’’.
Awali, akizungumza wakati akieleza malengo ya warsha hiyo, Kaimu Katibu Mtendaji wa TEITI Mariam Mgaya ameeleza sababu za Tanzania kujiunga na Mpango wa Kimataifa wa kuhamasisha Uwazi na Uwajibikaji katika Sekta ya uziduaji, yaani uchimbaji wa rasilimali za madini, mafuta na gesi asilia - (Extractive Industries Transparency Initiative) (EITI).
Amesema pamoja na kuhakiki mapato yanayotakiwa kulipwa kwa serikali, pia, ilikusudia kutoa nafasi kwa wananchi kujua kile ambacho Serikali inakipata kupitia rasilimali za madini, mafuta na gesi asilia, kutoa nafasi kwa wananchi kuhoji, kupunguza mianya ya rushwa na kuvutia uwekezaji kutokana na kuwekwa wazi kwa taarifa.
Mgaya amezitaja sababu nyingine kuwa ni pamoja na kuongeza mapato ya Serikali, kutoa nafasi kwa wananchi kushiriki katika shughuli zinazohusisha rasilimali hizo na kujenga imani ya Serikali kwa wananchi.
Amesema tangu Tanzania ijunge na umoja huo, tayari TEITI imekamilisha na kutoa ripoti 12 zenye takwimu za malipo ya kampuni za madini na gesi asilia kwa kipindi cha Julai 1, 2008 hadi Juni 2020.
Ameongeza kwamba, umoja huo una jumla ya wanachama 57 kidunia huku nchi za Afrika zikiwa 28 Tanzania ikiwa miongoni mwa nchi hizo.
Naye, Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro Joseph Mtataiko akizungumza katika ufunguzi huo umesema imekuwa ni wakati muafaka kwa Taasisi hiyo kutoa mafunzo hayo hususan wajibu wa kampuni kwa jamii zinazozunguka migodi na kueleza kuwa, kwa upande wa Mji Mdogo wa Mirerani bado wananchi hawajanufaika ipasavyo na uwepo wa kampuni za madini zinazofanya shughuli zake katika mji huo.
TEITI Office Dodoma
Postal Address: S.L.P 361 Kikuyu Ave.
Telephone: +255688386546
Mobile: +255688386546
Email: info@teiti.go.tz
Haki Miliki ©2017 TEITI .Haki zote Zimehifandiwa