Zikiwa zimetimia Siku 100 tangu ateuliwe na kuapishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan Februari 27, 2023 kuiongoza Wizara ya Madini, Juni 7, 2023, Katibu Mkuu Kheri Mahimbali akizungumza na Watumishi wa Wizara, aliwaeleza Mikakati Kabambe inayolenga kuifanya Sekta ya Madini Kuzalisha Zaidi.
Mahimbali alibainisha mikakati mbalimbali inayolenga kuifungamanisha Sekta ya madini na sekta nyingine kubwa kiuchumi ili ikuze uchumi, ichangie zaidi fedha za kigeni na iongeze mchango wake katika Pato la Taifa.
Mahimbali aliyataja maeneo ambayo tayari wizara imeanza kuweka msukumo na kuimarisha uhusiano katika utekelezaji wake ni pamoja Kilimo, Nishati, Mawasiliano na kueleza kwamba, kama taifa linayo madini ambayo yanaweza kutumika kuzalisha mbolea suala ambalo litapunguza gharama ya kuagiza mbolea kutoka nje na kusema kuwa, zaidi ya shilingi bilioni 700 zinatumika kununua mbolea kutoka nje.
Alitaja eneo lingine kuwa ni kuhakikisha huduma ya nishati inafika katika maeneo ya migodi ili kuongeza uzalishaji wa madini na kuwawezesha wachimbaji kuchimba kwa tija.
Akieleza uhusiano wa wizara na sekta nyingine katika kuboresha mazingira ya shughuli za uchimbaji alisema, kutokana na ushirikiano ambao umefanywa na wizara kwa kushirikiana na Wizara ya Nishati, umewezesha Mgodi wa dhahabu wa STAMIGOLD wa Biharamulo ulio chini ya Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kufikiwa na huduma ya nishati ya umeme na hivyo kupunguza gharama za uzalishaji.
Pia, amesema baada ya STAMIGOLD, Mgodi wa kuzalisha dhahabu wa Geita ambao umekua ukitumia gharama kubwa za uzalishaji kutokana na kukosa huduma hiyo muhimu uko mbioni kuunganishwa na nishati ya umeme.
Vilevile, alilitaja eneo lingine la kimkakati kuwa ni mawasiliano ambapo alisema lengo la wizara ni kuhakikisha migodi yote nchini inafikiwa huduma ya mawasiliano ya mtandao suala ambalo litaongeza tija kwenye shughuli za madini.
TEITI Office Dodoma
Postal Address: S.L.P 361 Kikuyu Ave.
Telephone: +255688386546
Mobile: +255688386546
Email: info@teiti.go.tz
Haki Miliki ©2017 TEITI .Haki zote Zimehifandiwa