TANZANIA YANG’ARA KATIKA UTEKELEZAJI WA SHUGHULI ZA UWAZI NA UWAJIBIKAJI KATIKA SEKTA YA MADINI
Arusha.
SERIKALI imesema itaendelea kuweka wazi taarifa za uwekezaji na mapato yanayopatikana katika sekta ya Madini, Mafuta na Gesi Asilia nchini kama Sheria inavyotaka na kwa kuzingatia vigezo vya Uwazi na Uwajibikaji vinavyosimamiwa na Asasi ya Kimataifa ya EITI.
Hayo yameelezwa leo Machi 13, 2025 na Mhe. Innocent Bashungwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi wakati akifungua akifungua mkutano wa 62 wa bodi ya Kimataifa ya Uwazi na Uwajibikaji (EITI), ulioanza jana jijini Arusha.
Waziri Bashungwa amesema wananchi wanapaswa kufuatilia na kujua mambo yanayoendelea katika sekta ya Madini, Mafuta na Gesi Asilia, Serikali itaendelea kuhakikisha kuwa mapato hayo yanawekwa wazi kwa lengo la kuimarisha uaminifu kwa wananchi.
Aidha, Waziri Bashungwa amesema "Kwa kuzingatia Tanzania ni mwanachama wa bodi ya EITI inayosimamia Uwazi na Uwajibikaji, Mwaka 2015 Serikali ilitunga Sheria ya kusimamia Uwazi na Uwajibikaji katika rasilimali Madini, Mafuta na Gesi Asilia, sura 447”.
Kwa upande wa Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde, amesema Taasisi ya TEITI inayosimamia Uwazi na Uwajibikaji nchini, imekuwa ikifanya vizuri kazi yake ambapo taarifa ya mwisho imeonyesha Serikali imeendelea kufanya vizuri katika kuweka Uwazi na Uwajibikaji wa taarifa za mapato yanayopatikana katika sekta hizo.
"Watu wengi wamekuwa wakitamani kuona nchi yetu inanufaikaje na rasilimali zilizopo kwenye Madini, Mafuta na Gesi Asilia, kwa kupitia utaratibu huu wa Uwazi na Uwajibikaji ambao nunawekwa kwenye taarifa za mapato ndipo wananchi wetu wanaweza kufahamu jinsi rasilimali hizo zinavyoweza kututajirisha, " amesema.
Amesema chini ya Serikali ya Awamu ya Sita ya Rais Samia Suluhu Hassan sekta ya Madini, Mafuta na Gesi Asilia zimekuwa zikifanya vizuri na hivyo kuvutia wawekezaji wengi zaidi Nchini. Pamoja na hayo, Mhe. Waziri ameeleza kuwa kufanyika kwa mkutano wa 62 wa Bodi ya Kimataifa - EITI hapa Nchini ni matokeo mazuri ya Tathmini ya EITI iliyofanyika mwaka 2023 ambapo Bodi hiyo ilipongeza juhudi za Serikali ya Tanzania na wadau mbalimbali katika kufanikisha utekelezaji wa shughuli za EITI hapa Nchini.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Taasisi ya Uwazi na Uwajibikaji Nchini - (TEITI), CPA. Ludovick Utouh amesema bodi hiyo inakutana kwa mara ya kwanza Tanzania tangu Tanzania kujiunga mwaka 2009.
Mkutano huo umehudhuriwa na washiriki zaidi ya mia moja ikiwa ni wajumbe wa Bodi ya EITI kutoka Mataifa mbalimbali Duniani ikijumuisha wawakilishi wa Kampuni kubwa zinazojihusisha na shughuli za uchimbaji na utafutaji wa Rasilimali Madini, Mafuta na Gesi Asilia, Asasi za Kiraia zinazojihusisha na shughuli za Uziduaji, Sekretarieti ya EITI na wawakilishi wa nchi wanachama wa EITI Duniani.
Taasisi ya Kimataifa ya Uwazi na Uwajibikaji (EITI), yenye makao Makuu Oslo Nchini Norway ina jumla ya nchi wanachama 57 Duniani.
TEITI Office Dodoma
Postal Address: S.L.P 361 Kikuyu Ave.
Telephone: +255688386546
Mobile: +255688386546
Email: info@teiti.go.tz
Copyright ©2016 GWF . All rights reserved.