TANZANIA YASHIRIKI KATIKA MKUTANO WA KIMATAIFA WA EITI NCHINI SENEGAL
Ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa umeshiriki katika Mkutano wa Kimaifa wa Uwazi na Uwajibikaji katika rasilimali Madini, Mafuta na Gesi asilia unaofanyika nchini Senegal kuanzia tarehe 13 – 14 Juni, 2023, Mkutano huo umeandaliwa na Asasi ya Kimataifa ya EITI ambapo Tanzania ni mwanachama wa Asasi hiyo.
Lengo la Mkutano huo ni kuunganisha nchi wanachama wa EITI (zaidi ya nchi 50 duniani) kujadili changamoto na mafanikio katika utekelezaji wa vigezo vya kimataifa vya EITI. Aidha, Mkutano huu ni fursa ya kutoa mapendekezo yatakayowezesha kuboresha shughuli za Uwazi na Uwajibikaji katika usimamizi wa rasilimali Madini, Mafuta na Gesi Asilia duniani.
Aidha, Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ameshiriki katika ufunguzi wa mkutano huo kwa njia ya mtandao na kutoa hotuba yake juu ya utekelezaji wa shughuli za Uwazi na Uwajibikaji katika Sekta ya Madini, Mafuta na Gesi Asilia hapa nchini. Katika hotuba hiyo Mhe. Rais alieleza kuwa Tanzania inaendelea kutekeleza vigezo vya kimataifa vya uwazi na uwajibikaji kikamilifu ili kuongeza manufaa yanayotokana na shughuli za utafutaji na uchimbaji wa rasilimali hizo nchini. Aidha, alieleza kuwa hadi sasa Tanzania imeweka wazi ripoti kumi na mbili (12) za ulinganishi wa malipo ya kampuni za madini, mafuta na gesi asilia na mapato ya serikali.
Mkutano huo pia umehudhuriwa na Kamishna wa Madini Dkt. Abdulrahman Mwanga; Mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Bw. Dunstan Kitandula, Mjumbe wa kamati ya kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Bi. Jesca Kishoa, Mwenyekiti wa kamati ya TEITI Bw. Ludovick Utouh, Mjumbe wa kamati ya TEITI Bw. Adam Anthony na Kaimu katibu Mtendaji wa TEITI Bi. Mariam Mgaya.
TEITI Office Dodoma
Postal Address: S.L.P 361 Kikuyu Ave.
Telephone: +255688386546
Mobile: +255688386546
Email: info@teiti.go.tz
Haki Miliki ©2017 TEITI .Haki zote Zimehifandiwa