TEITI YAKUTANA NA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA NISHATI NA MADINI
Na Tito Mselem Dodoma,
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Dunstan Kitandula ameendelea kuongoza Vikao vya Wizara ya Madini na Taasisi zake ambapo leo Januari 26, 2021, Kamati hiyo imeijadili Tume ya Madini na Taasisi ya Uhamasishaji, Uwazi na Uwajibikaji katika Rasilimali Madini, Matuta na Gesi Asilia (TEITI)
Katika kikao hicho, Kitandula ameipongeza Tume ya Madini na TEITI kwa kuonesha mwanga wa mafanikio na kuzitaka Taasisi hizo ziendelee kuboresha majukumu yake ili kuongeza ufanisi katika shughuli zake.
Akijibu swali la Mbunge wa Bahi, Kenneth Nollo, Naibu Waziri wa Madini Prof. Shukrani Manya, amesema, suala la milipuko ya madini (Rush) ni suala la dharura tu, lazima sehemu zote zenye mifumuko ya madini zilasimishwe kwa kupatiwa leseni ili kuepusha vurugu na changamoto zinazoweza kujitokeza.
“Rush ni kitu cha mpito hakitaachiwa kiendelee kwa muda mrefu na badala yake maeneo yote yenye rush yarasimishwe ili yasaidie kwenye suala la ushirikishwaji wa watanzania kwenye rasilimali ya madini ambayo watanzania wote wanatakiwa kunufaika nayo,” amesema Prof. Manya.
Naye, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Prof. Simon Msanjila, amesema, Wizara ya Madini inaendelea kutoa elimu kwa umma kupitia njia mbalimbali ili kuhakikisha umma unapata taarifa sahihi na kutambua Sheria ya Madini ambapo kwasasa watu wengi wanachanganya kati ya haki ya ardhi na haki ya Madini.
Akiwakilisha Taarifa ya Tume ya Madini, Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini Mhandisi Yahya Samamba amesema, kiwango cha makusanyo ya Maduhuli ya Serikali kilipanda kutoka Sh. bilioni 346.275 zilizokusanywa mwaka 2018/19 na kufikia Sh. bilioni 528.24 mwaka 2019/20.
Imeelezwa kuwa Tume ya Madini imepanga kukusanya jumla ya Sh. 526, 722, 000 sawa na Sh. 263,361,273,500 kwa kipindi cha miezi sita (Julai-Desemba) ambapo mpaka sasa Tume ya Madini imekusanya jumla ya Sh. 317,498,886,008.21 sawa na asilimia 60.27 ya lengo la nusu mwaka 2020/21.
“Tume ya Madini iliendelea kusimamia shughuli zote za uthaminishaji madini nchini na kushiriki katika minada ya madini, kufanya kaguzi za kifedha za mapitio ya kodi, kuandaa bei elekezi na usimamizi wa shughuli za maabara,” alisema Mhandisi Samamba.
Kwa upande wake, Kaimu Katibu Mtendaji wa TEITI Marium Mgaya, amesema, TEITI imefanikiwa kutoa ripoti kumi (10) kwa mwaka wa fedha 2008/09 hadi 2017/18, ambapo ripoti hizo zinaonesha kuwa Serikali imepokea kiasi cha Dola bilioni 3.51 za Marekani kutoka katika kodi mbalimbali zilizolipwa na kampuni za madini, mafuta na gesi asilia.
“TEITI itaendelea kuhakikisha kuwa Serikali inaboresha mifumo ya uwazi na uwajibikaji katika usimamizi wa rasilimali madini, mafuta na gesi asilia ili kuongeza ukusanyaji wa mapato na manufaa yatokanayo na shughuli za utafutaji na uchimbaji wa rasilimali hizo nchini,” alisema Mgaya.
TEITI Office Dodoma
Postal Address: S.L.P 361 Kikuyu Ave.
Telephone: +255688386546
Mobile: +255688386546
Email: info@teiti.go.tz
Haki Miliki ©2017 TEITI .Haki zote Zimehifandiwa