TEITI YAWAPIGA MSASA MADIWANI, ASASI ZA KIRAIA NA VIONGOZI WA HALMASHAURI KILWA MASOKO
Taasisi ya Uhamasishaji Uwazi na Uwajibikaji Katika Rasilimali za Madini, Mafuta na Gesi Asilia (TEITI) imewapatia Elimu Madiwani, Waeka Hazina wa Halmashauri ya Kilwa, Washiriki kutoka Asasi za Kiraia, Wachimbaji Wadogo wa Madini na Waandishi wa Vyombo katika warsha iliyofanyika katika ukumbi wa PEC Kwa Sultan uliopo kata ya Kilwa Masoko Wilayani Kilwa Mkoa wa Lindi tarehe 21 Juni, 2022.
Akifungua warsha hiyo Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kilwa Masoko Ndg. Swahaba Matajiri alieleza kuwa tayari taarifa za TEITI zinahakikiwa na kutumika kwa manufaa ya wananchi wote. Huku kampuni zinazofanya shughuli za utafiti na uchimbaji wa Madini, Mafuta na Gesi Asilia zinawajibika kuweka wazi taarifa za mapato hayo kulingana na sheria inavyoelekeza.
Ndg. Matajiri alisisitiza kuwa, wadau watumie warsha hiyo, kujifunza, kuchambua, kujadiliana na kushauriana juu ya namna bora ya kuelewa na kutumia takwimu zinazochapishwa na TEITI kila mwaka juu ya aina na kiasi kinacholipwa na kampuni za Madini, Mafuta na Gesi Asilia, na kupokelewa na Serikali kwa mujibu wa sheria za nchi.
Matajiri alisema, warsha hii ni muhimu na kielelezo kikubwa katika kufanikisha na kuboresha suala zima la uwazi na uwajibikaji katika Sekta ya uziduaji nchini kwani Serikali ya Awamu ya Sita ina dhamira ya dhati kuona kwamba sekta hizo zinawanufaisha wananchi na kuhakikisha kwamba Serikali inapata mapato stahiki.
"Ni matumaini yangu kuwa wadau kupitia fursa hii watajifunza na kuibua mijadala ambayo itasaidia kuboresha Sekta ya Uziduaji ikiwemo ushiriki wa Wananchi katika kutoa huduma na bidhaa kwenye Migodi (CSR), pia, uwajibikaji wa Kampuni kwa Jamii ndiyo ambayo wadau hao wanapaswa kujifunza na Serikali inapenda kuona yanafanyiwa kazi na kufahamika vizuri miongoni mwa Wadau hao. Kila mwekezaji ahakikishe anakuwa na mpango mahususi unaobainisha kwamba yeye katika mwaka wake wa fedha anatenga kiasi kadhaa kama sehemu ya huduma kwa Jamii na taarifa hizo zinaenda kwenye Halmashauri husika ili kuweza kufanyiwa kazi kupitia Baraza lake la Madiwani kutokana na mchango huo uliotolewa na Mwekezaji katika Sekta hiyo”, alisema.
Aidha, uchambuzi wa ripoti ya TEITI utasaidia Wananchi kufahamu kwa uhakika aina na kiasi cha kodi au tozo zinazolipwa na Kampuni Serikalini, gharama uwekezaji na uzalishaji katika sekta hizo kwa hiyo ripoti za TEITI ni nyaraka na nyenzo muhimu kwani zinaweka wazi takwimu mbalimbali kuhusu ripoti na tozo zingine zinazolipwa Serikalini na Kampuni za rasilimali hizo kwani zikiwafikia Wananchi kwa muda unaotakiwa zitasaidia kujibu maswali mbalimbali kuhusu Sekta hiyo Nchini.
Naye, Bw. Erick Ketagory mwakilishi wa Kaimu Katibu Mtendaji wa TEITI alisema kuwa, tayari mpaka sasa TEITI imeshakamilisha na kuweka wazi ripoti 11 zenye takwimu za Kampuni za Madini, Mafuta na Gesi Asilia. Nchi wanachama wa Asasi ya EITI hutakiwa kuweka wazi malipo ya kodi na mapato yaliyofanywa na Kampuni za Madini, Mafuta na Gesi Asilia kwa Serikali Kuu na katika Halmashauri kwa kila mwaka.
Naye, Mhe. Eston Paul Ngilangwa, Mkurugenzi wa Halmashauri ameipongeza Serikali kwa kuona umuhimu wa kutoa elimu hiyo kwa Jamii Mkoani humo kwani wadau hao wataenda kuwa mabalozi wazuri kwa Wachimbaji wenzao na Jamii kwa ujumla kuhusu elimu hiyo ambayo wameipata kupitia mafunzo hayo ili kuleta uelewa zaidi kwa jamii yao kuhusu majukumu ya TEITI hasa suala la uwazi na uwajibikaji.
Nao Madiwani ambao ni walengwa wakuu wa warsha hii wakipata elimu kwa niaba ya wananchi, wameipongeza TEITI kwa elimu nzuri huku wakikiri kutofahamu mengi hapo awali kuhusu Kampuni za Madini huku wakidai kuamka na ari mpya katika kufuatilia miradi, kuwasilisha taarifa katika Halmashauri na kuhimiza uwajibikaji hasa jambo la Kampuni hizo Kurudisha kwa wananchi (CSR) kwa utaratibu jambo ambalo Kampuni nyingi wilayani Kilwa zimekuwa hazitekelezi.
Hadi sasa Tanzania imechapisha na kutoa ripoti kumi na moja kwa kipindi cha Julai 1, 2008 hadi Juni 30, 2019 zinazolinganisha kodi na malipo mengine yaliyofanywa na kampuni za Madini, Mafuta na Gesi Asilia kwa Serikali Kuu na katika Halmashauri ambazo zinapokea tozo (Service Levy).
TEITI Office Dodoma
Postal Address: S.L.P 361 Kikuyu Ave.
Telephone: +255688386546
Mobile: +255688386546
Email: info@teiti.go.tz
Haki Miliki ©2017 TEITI .Haki zote Zimehifandiwa