TEITI YAWAPIGA MSASA MADIWANI, ASASI ZA KIRAIA NA VIONGOZI WA HALMASHAURI MTWARA
Taasisi ya Uhamasishaji Uwazi na Uwajibikaji katika Rasilimali za Madini, Mafuta, na Gesi Asilia (TEITI) ina wajibu wa kuhakikisha kuwa, mapato ya tasnia ya uziduaji yanahakikiwa na kutumika kwa manufaa ya wananchi wote na ina jukumu la kuhakikisha Kampuni zinazofanya shughuli za utafutaji na uchimbaji wa madini, mafuta na gesi asilia zinaweka wazi taarifa za mapato hayo.
Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri Dkt. Steven Kiruswa wakati akifungua warsha ya kuelimisha Madiwani, Asasi za Kiraia na Viongozi wa Halmashauri juu ya matumizi ya Takwimu zinazotolewa katika Ripoti TEITI iliyofanyika katika ukumbi wa Mkuu wa Mkoa wa Mtwara.
Aidha, Dkt. Kiruswa amesema kuwa, tukio hilo ni muhimu na ni kielelezo kikubwa katika kufanikisha na kuboresha suala zima la uwazi na uwajibikaji katika Sekta ya uziduaji Nchini kwani Serikali ya awamu ya sita ina dhamira ya dhati kuona kwamba Sekta hizo zinawanufaisha Wananchi na kuhakikisha kwamba Serikali inapata mapato stahiki.
Dkt. Kiruswa amesema kuwa, ni matumaini yake kuwa Wadau kupitia fursa hiyo watajifunza na kuibua mijadala ambayo itasaidia kuboresha Sekta hiyo ya uziduaji ikiwemo ushiriki wa Wananchi katika kutoa huduma na bidhaa kwenye Migodi lakini pia uwajibikaji wa Kampuni kwa Jamii kwani hayo ndiyo ambayo Wadau hao wanapaswa kujifunza na Serikali inapenda kuona yanafanyiwa kazi na kufahamika vizuri miongoni mwa Wadau hao.
“Kila mwekezaji ahakikisha anakuwa na mpango mahususi unaobainisha kwamba yeye katika mwaka wake wa fedha anatenga kiasi kadhaa kama sehemu ya huduma kwa Jamii na taarifa hizo zinaenda kwenye Halmashauri husika ili kuweza kulifanyika kazi kupitia Baraza lake la Madiwani kutokana na mchango huo uliotolewa na Mwekezaji katika Sektka hiyo”, amesema Dkt. Kiruswa.
Amesema kuwa, uchambuzi wa ripoti ya TEITI utasaidia Wananchi kufahamu kwa uhakika aina na kiasi cha kodi au tozo zinazolipwa na Kampuni Serikalini, gharama uwekezaji na uzalishaji katika sekta hizo kwa hiyo ripoti za TEITI ni nyaraka na nyenzo muhumi kwani zinaweka wazi takwimu mbalimbali kuhusu ripoti na tozo zingine linazolipwa Serikalini na Kampuni za rasilimali hizo kwani zikiwafikia Wananchi kwa muda unaotakiwa zitasaidia kujibu maswali kuhusu Sekta hiyo Nchini.
Pamoja na mambo mengine Dkt. Kiruswa alipata fursa ya kutembelea Bandari ya Mkoa wa Mtwara ambapo madini ya makaa ya mawe yanahifadhiwa tayari kwa kusafirishwa nje ya nchi na pia, alitembelea Kiwanda cha kuzalisha saruji cha Dangote.
“Niwaombe kila mmoja wetu ifikapo mwezi Agosti, 2022 tujiandae kuhesabiwa. Sense ina manufaa makubwa kwa maendeleo ya nchi kwani bila kuwa na Takwimu sahihi mipango haiwezi kuwa sahihi", Dkt Kiruswa wakati akihitimisha hotuba yake.
Kaimu Katibu Mtendaji wa TEITI Mariam Mgaya amesema kuwa, tayari mpaka sasa TEITI imeshakamilisha na kuweka wazi ripoti 11 yenye takwimu za Kampuni za Madini, Mafuta na Gesi Asilia kwa kipindi cha Julai 1, 2008 hadi Juni 30, 2019 na katika ripoti hizo Serikali imekusanya Bilioni 3.78 Dola za Kimarekani ambapo katika Mwaka wa Fedha 2019/2020 ipo kwenye hatua za mwisho na zitawekwa wazi kabla ya Juni mwaka huu 2020/22.
Kwa upande wake, Afisa Madini Mkazi Mkoa wa Mtwara Ephraim Mushi amesema Mkoa wa Mtwara una madini ya dhahabu ya kutosho hasa maeneo ya Masasi na
Nanyumbu ila kikubwa ameomba watalaam kuja kuufanyia utafiti mkoa huo ili kujua wingi wa dhahabu iliyopo kwenye maeneo mengine lakini pia amezungumzia uwepo mdogo wa uwekezaji katika madini ya dhahabu katika Mkoa huo.
Naye, Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Dunstan Kyobya ameiomba Serikali kupitia Wizara ya Madini kuwezesha uwekezaji wa kiwanda cha chumvi mkoa humo kutokana na mkoa kuwa na madini ya Chumvi ya kutosha na hawana tekinolojia, uelewa wa kutosha lakini pia kuongeza uzalishaji, ajira na kipato kwa Serikali.
Pia, Kyobya ameipongeza Serikali kwa kuona umuhimu wa kutoa elimu hiyo kwa Jamii Mkoani humo kwani wadau hao wataenda kuwa mabalozi wazuri kwa Wachimbaji wenzao na Jamii kwa ujumla kuhusu elimu hiyo ambayo awameipata kupitia mafunzo hayo ili kuleta uelewa zaidi kwa jamii yao kuhusu majukumu ya TEITI hasa suala la uwazi na uwajibikaji.
TEITI Office Dodoma
Postal Address: S.L.P 361 Kikuyu Ave.
Telephone: +255688386546
Mobile: +255688386546
Email: info@teiti.go.tz
Haki Miliki ©2017 TEITI .Haki zote Zimehifandiwa