TUNAPATA USHIRIKIANO MKUBWA KUTOKA SERIKALINI, WANANCHI – WDL
DKT. KIRUSWA AMWAKIKISHIA UTATUZI WA CHANGAMOTO
CapeTown
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Petra Diamonds na Mwenyekiti wa Kampuni ya Williamson Diamonds Limited, inayofanya shughuli za Uchimbaji wa Madini ya Almasi Mwadui Richard Duffy, ameishukuru Serikali ya Tanzania kufuatia ushirikiano ambao inaendelea kuupata kwenye uwekezaji wa kampuni hiyo nchini.
Ameongeza kuwa, katika kipindi cha miaka mitano, kampuni hiyo imeshuhudia mabadiliko makubwa yenye tija yakihusisha mahusiano mazuri ambayo kampuni hiyo inayapata kutoka kwenye jamii inayozunguka mgodi huo.
Amesema Mgodi huo utaendelea kufanya shughuli zake kwa kushirikiana na jamii inayouzunguka na kuongeza kwamba, ni moja ya migodi ya kiwango cha juu duniani.
Aidha, Duffy amemweleza Naibu Waziri kuhusu changamoto ambazo mgodi huo inakabiliana nazo na kuiomba Serikali kusaidia ikiwemo nishati ya umeme na masuala ya kikodi kuchukua muda mrefu kupatiwa ufumbuzi.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa amesema Serikali imedhamiria kuendelea kuweka mazingira rafiki ili kuwezesha shughuli za madini kufanyika na kuleta matokeo kutokana na umuhimu wa Sekta ya Madini katika maendeleo ya kiuchumi.
Aidha, Dkt. Kiruswa amemweleza Mkurugenzi huyo kuhusu hatua mbalimbali ambazo Serikali inaendelea kuzichukua kuboresha mazingira ya uwekezaji ikiwemo ujenzi wa Bwawa la Julius Nyerere ambalo kukamilika kwake litazalisha Megawati 2,115.
Pia, Dkt. Kiruswa ametoa ushauri kwa kampuni za madini kuwa na utaratibu wa kukutana na vyombo vya habari ili kutoa ufafanuzi wa taarifa za utekelezaji Wa miradi ili kuweka uelewa wa pamoja Kwa wananchi na kuongeza kuwa Wizara Iko tayari kushirikia na kampuni hizo.
Mgodi wa Mwadui ni wa ubia kati ya Kampuni ya Williamson Diamonds yenye umiliki wa hisa zipatazo 63 na Serikali inamiliki asilimia 37 kutoka asilimia 25 za awali.
Katika hatua nyingine, Viongozi na Watendaji wa Wizara wameendekea kukutana na kampuni mbalimbali.
TEITI Office Dodoma
Postal Address: S.L.P 361 Kikuyu Ave.
Telephone: +255688386546
Mobile: +255688386546
Email: info@teiti.go.tz
Haki Miliki ©2017 TEITI .Haki zote Zimehifandiwa