Utoaji Leseni kwa Kampuni za Nyati Mineral Sands, Kiwanda cha Uchenjuaji wa Madini ya Metali Kukuza Uchumi Nchini
Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde amesema kuwa utoaji wa leseni za madini kwa kampuni za Nyati Mineral Sands na Kampuni ya Tembo Nickel Refining yenye kiwanda cha uchenjuaji wa madini ya metali, unatarajiwa kukuza uchumi wa nchi kupitia ukusanyaji wa mapato, kodi na tozo mbalimbali, kutoa ajira na kuongeza fursa za biashara.
Ameyasema hayo leo Machi 21, 2024 jijini Dodoma katikaHafla ya kukabidhi leseni hizo na kufafanua kuwa kabla ya leseni hizo mbili kutolewa leo, nchi ilikuwa na jumla ya leseni 19 za uchimbaji mkubwa wa madini na leseni za viwanda vya usafishaji wa madini 6, hivyo kwa kutolewa kwa leseni hio kunaongeza idadi ya leseni za uchimbaji mkubwa kufikia 20 na leseni za viwanda vya usafishaji wa madini kufikia 7.
"Katika kampuni ya ubia ya Nyati Mineral Sands Limited zitawekezwa dola za marekani milioni 127.7 na mradi utaanza kuzalisha faida baada ya miaka 4 na miezi 6. Kutokana na uwekezaji huu Serikali itanufaika na kukusanya mapato takribani dola za marekani milioni 437.96 kutokana na gawio la hisa za Serikali, kodi na tozo mbalimbali, fursa za ajira za moja kwa moja zipatazo 150 ikijumuisha ajira 140 za Watanzania na 10 za wageni, kuongezeka kwa fursa za biashara, na kuimarika kwa hali ya kiuchumi na ustawi wa jamii kutokana na uwepo wa miradi ya huduma za jamii zitakazotolewa kupitia utaratibu wa Corporate Social Responsibility (CSR)", alisema Mhe. Mavunde.
Ameongeza kuwa, Wizara katika kuhakikisha kuwa inatatua changamoto zinazojitokeza kwenye sekta ya madini nchini, inaendelea kufanya mazungumzo na wawekezaji wa nyanja mbalimbali ikiwemo utafutaji, uchimbaji na ujenzi wa viwanda vya usafishaji madini ili kwa njia ya kuingia ubia na Watanzania, hivyo kuongeza wigo wa upatikanaji wa mitaji, utaalam pamoja na uhaulishaji wa teknolojia.
"Kiwanda cha usafishaji wa madini kitawekezwa kwa dola za marekani milioni 500 ambapo kiwanda hicho kinatarajiwa kutatua changamoto iliyokuwepo kwa wachimbaji wa madini nchini kulazimika kusafirisha makinikia ya metali kwenda kwenye viwanda vya nje ya nchi.
TEITI Office Dodoma
Postal Address: S.L.P 361 Kikuyu Ave.
Telephone: +255688386546
Mobile: +255688386546
Email: info@teiti.go.tz
Haki Miliki ©2017 TEITI .Haki zote Zimehifandiwa