Waziri Biteko azindua rasmi Kamati na ripoti za TEITI
Na Tito Mselem na Godwin Masabala Dar es Salaam,
Waziri wa Madini Doto Biteko amezindua Kamati Mpya ya Uhamasishaji, Uwazi na Uwajibikaji katika Rasilimali za Madini, Mafuta na Gesi Asilia (TEITI) kwa Kipindi cha 2019-2022 na ripoti mbili za TEITI kwa mwaka 2016/17 na 2017/18 ambapo kamati hiyo itakuwa na jukumu la kuhakikisha kuwa mapato ya Sekta ya Uziduaji yanayopaswa kuwasilishwa Serikalini yanahakikiwa na kutumika kwa manufaa ya wananchi wote.
Uzinduzi huo umefanyika juni 26, 2020 katika ukumbi wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam wenye lengo la kuweka taarifa wazi kwa ajili ya wananchi na wadau mbalimbali kutumia takwimu zinazopatikana katika ripoti hiyo ili kuboresha na kuongeza mchango wa Sekta ya Madini, Mafuta na Gesi Asilia katika pato la taifa.
Imeleezwa kuwa, Tanzania ilijiunga katika mpango wa kimataifa wa kuhamasisha Uwazi na Uwajibikaji katika Sekta ya Uchimbaji wa Rasilimali Madini mwaka 2009 lengo lake kuu ikiwa ni kuhakikisha kwamba mapato yanayotakiwa kulipwa Serikalini kutoka katika Sekta ya Uziduaji yanapatikana na yanawekwa wazi kwa wananchi.
Waziri Biteko amesema kuwa mantiki ya falsafa ya Uwazi na Uwajibikaji kwenye Sekta ya uziduaji inatokana na Ibara ya 8 (1) (c) na Ibara 27 (1) & (2) za Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ambapo ibara hizi zinazungumzia Serikali kuwajibika kwa wananchi wake na kuwa rasilimali zote za nchi zitatunzwa na wananchi wote kwa manufaa ya wote.
“Napenda kuwahakikishia kuwa Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Uongozi wa Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ina dhamira ya dhati kabisa kuona kwamba Sekta ya Uziduaji inawanufaisha watanzania wote kwa kuhakikisha kwamba Serikali inapata mapato yake stahiki na wananchi wanashiriki kikamilifu katika usimamizi wa rasilimali hizo,” alisema Waziri Biteko.
Wakati huo huo Waziri Biteko ameitaka kamati hiyo kuwa wasimamizi wa kuhakikisha Serikali inaboresha Uwazi na Uwajibikaji katika usimamizi wa Sekta ya uziduaji hususan kwenye utoaji wa Leseni na Mikataba, usimamizi na uendeshaji wa Kampuni, ukusanyaji wa Mapato na mgawanyo wa mapato na matumizi.
“Naomba mtambue kuwa mmepewa mamlaka makubwa na Imani kubwa sana ya kulinda maslahi ya nchi kwa kusimamia Sheria ya Uwazi na Uwajibikaji katika Rasilimali za Madini, Mafuta na Gesi Asilia Tanzania ni Imani yangu kuwa mna nafasi kubwa ya kusaidia Serikali katika agenda yake ya kuboresha Sekta hii muhimu kwa kuainisha njia za kuboresha usimamizi wa Sekta, kuvutia wawekezaji, kuongeza pato la Serikali na kujenga imani kwa wadau wa sekta hii,” alisema Waziri Biteko.
Waziri Biteko aliongeza kuwa, Serikali na wananchi wana matarajio makubwa kuwa kamati itahakikisha kunakuwa na Uwazi na Uwajibikaji katika usimamizi wa rasilimali za nchi, lengo ni kuzuia udanganyifu na ukwepaji wa ulipaji wa kodi kulingana na sheria za nchi yetu ili hatimaye vizazi vijavyo vinufaike na utajiri wa Rasilimali za Madini, Mafuta na Gesi Asilia vilivyopo nchini,
Aidha, Waziri Biteko, ameitaka kamati hiyo mpya iibadilishe TEITI ambayo haijulikani kwa wananchi walio wengi na kuwa TEITI ambayo inajulikana na kila Mtanzania.
Pia, Waziri Biteko amezitaka Kampuni zilizoshindwa kutoa ushirikiano kwa kamati hiyo zichukuliwe hatua kwani kamati hiyo ipo kwa mujibu wa sheria na kampuni zote za madini, mafuta na gesi zinatakiwa kutoa taarifa zake kwa kamati hiyo.
TEITI Office Dodoma
Postal Address: S.L.P 361 Kikuyu Ave.
Telephone: +255688386546
Mobile: +255688386546
Email: info@teiti.go.tz
Haki Miliki ©2017 TEITI .Haki zote Zimehifandiwa