Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa leo Septemba 22, 2019 amefungua Maonesho ya Teknolojia na Uwekezaji kwenye Sekta ya Madini yaliyoanza tarehe 20 Septemba, 2019 na kutarajiwa kumalizika tarehe 29 Septemba, 2019.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa maonesho hayo, Waziri Mkuu Majaliwa ametoa pongezi kwa Wizara ya Madini na Tume ya Madini kwa kuboresha shughuli za madini kupitia kuongeza ajira na vitendea kazi kama vile magari kama njia mojawapo ya kuboresha ukusanyaji wa maduhuli.
Akielezea mafanikio ya Soko la Madini Geita tangu kuanzishwa kwake Majaliwa amesema kuwa ni pamoja na kuongezeka kwa uzalishaji wa dhahabu kutoka takribani kilo 100 hadi kilo 200 na zaidi kwa mwezi na kusisitiza kuwa, tangu kuanzishwa kwa soko la madini la Geita kiasi cha kilo 1,573 zimezalishwa na kuuzwa.
Katika hatua nyingine, ameitaka Tume ya Madini kuongeza kasi kwenye ukusanyaji wa maduhuli ili Sekta ya Madini iwe na mchango mkubwa kwenye ukuaji wa uchumi wa nchi .
Aidha, amewataka wachimbaji na wafanyabiashara wa madini kuyatumia vyema masoko ya madini yaliyoanzishwa nchini na kuwataka wakuu wa mikoa na wilaya kuhakikisha yanalindwa.
Pia, amewataka wachimbaji wa madini kutumia tafiti zinazofanywa na Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini (GST) kubaini maeneo yanye madini na kuanza kuchimba ili kuepuka uchimbaji wa kubahatisha.
Amesema serikali itaendelea kuboresha Sheria na Kanuni ili kuleta tija zaidi na hivyo kuwataka wananchi kuchangamkia fursa zilizopo kwenye sekta ya madini ikiwemo kutoa taarifa kwenye vyombo vya udhibiti.
Katika hatua nyingine Waziri Mkuu Majaliwa amewataka wachimbaji wadogo wa madini kuachana na matumizi ya zebaki na badala yake watumie njia nyingine mbadala kulingana na miongozo mbalimbali inayotolewa na Wizara ya Madini pamoja na Tume ya Madini.
Akizungumzia nafasi ya sekta ya madini katika kuchochea ukuaji wa viwanda, Waziri wa Madini, Doto Biteko amesema kwamba hadi sasa wizara kupitia Tume ya Madini imekwishatoa leseni mbili za usafishaji wa madini (Refinery Licence) moja ikiwa mkoani Dodoma na nyingine mkoani Geita.
Ameongeza kuwa, Wizara ya Madini kupitia Tume ya Madini imetoa leseni nne za uyeyushaji wa madini ya Shaba na Bati ( Smelting Licence ).
Kuhusu changamoto ya usafirishaji nje madini ya bati amesema Wizara kwa kushirikiana na Jumuiya ya Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR) zipo katika hatua ya mwisho kuwezesha upatikanaji wa Hati ya kusafirisha madini ya bati nje ya nchi na kuongeza kwamba, hadi kufikia mwezi Desemba mwaka huu, hati hiyo itakuwa tayari.
Akizungumzia uanzishwaji wa masoko ya madini, Waziri Biteko amesema masoko hayo yameleta matokeo chanya huku nidhamu ya watanzania kusimamia masoko na rasilimali ikiwa imeongezeka hali ambayo imepelekea baadhi ya nchi zikiwemo za Kongo, Zambia na Msumbiji kutaka kuyatumia masoko ya madini yaliyoanzishwa katika mikoa mbalimbali nchini.
‘’ Wanaotaka kuhujumu masoko waache. Ukifanya hivyo utaambulia vitu viwili tu, kufilisiwa na kufungwa jela,’’ amesisitiza Waziri Biteko.
Pia, Waziri Biteko amebainisha kuwa, wadau wa madini nchini hawakatazwi kuingiza madini nchini kutoka nchi mbalimbali zikiwemo sampuli isipokuwa tu madini yote yanayopelekwa nje ya nchi ni lazima yazingatie sheria na taratibu.
Katika hatua nyingine, Waziri Biteko ameupongeza Mkoa wa Geita kwa kuwa kinara kwenye usimamizi wa fedha zinazotokana na mpango wa utoaji wa huduma kwa wananchi wanaozunguka kampuni za madini (CSR) na kuzitaka kuendelea kufuata sheria na taratibu zinazowekwa na serikali kwenye usimamizi wa sekta ya madini.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel amesema kuwa, tangu kuanzishwa kwa soko la madini mkoani humo, madini ya dhahabu yameanza kupatikana kwa wingi na kueleza kwamba kwa mwezi Agosti mwaka huu jumla ya kilo 504 zimeuzwa sokoni hapo, na kabla ya kuisha kwa mwezi Septemba tayari kilo 340 zimeuzwa sokoni.
Akizungumzia lengo la maonesho hayo Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi, Chacha Wambura amesema kuwa ni pamoja na kukuza teknolojia ya uchimbaji wa madini kwa wachimbaji wadogo na kutangaza fursa mbalimbali zilizopo katika mkoa wa Geita.
Katika hatua nyingine ikiwa ni sehemu ya ufunguzi wa maonesho hayo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amezindua mwongozo wa uwekezaji katika mkoa huo.
Maonesho hayo yemehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali wakiwemo Wakuu wa Mikoa jirani na Geita, Viongozi wa Wizara ya Madini na Tume ya Madini, Wawakilishi wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Taasisi za Kifedha, wadau mbalimbali wa madini na wananchi.
Kaulimbiu ya maonesho hayo ‘’Madini ni Chachu ya Ukuaji wa uchumi wa Viwanda. Tuwekeze kwenye Teknolojia bora ya Uzalishaji na Tuyatumie Masoko ya Madini’’
TEITI Office Dodoma
Postal Address: S.L.P 361 Kikuyu Ave.
Telephone: +255688386546
Mobile: +255688386546
Email: info@teiti.go.tz
Haki Miliki ©2017 TEITI .Haki zote Zimehifandiwa