YALIYOSEMWA NA MKUU WA MKOA WA GEITA MHANDISI ROBERT GABRIEL WAKATI AKIFUNGUA KONGAMANO LA KUJADILI SEKTA YA MADINI KATIKA MAONESHO YA TEKNOLOJIA NA UWEKEZAJI YANAYOENDELEA MKOANI GEITA
Asteria Muhozya, Greyson Mwase na Boaz Magizo,Geita
Tumejikuta tuna kundi kubwa la wachimbaji wadogo wa madini ambao hawana mitaji lakini wanataka maisha yao yabadilike. Ni kundi ambalo lina nguvu, hamasa ni kundi ambalo naliangalia sana.
Kwa jicho lingine naziangalia Taasisi za serikali kama GST, taasisi za fedha, nataka tuzungumze, wachimbaji wana maswali magumu, ardhi ipo, benki zipo, ipo haja ya kuwa na vikundi maalum tukaviangalia na tuviwezeshe.
Tumeanza kuandaa eneo Maalum la Maonesho lenye hadhi ya Kimataifa. Litaanza kutumika kwa biashara muhimu mwaka mzima hatutasubiri maonesho na litakidhi mahitaji yote. Atakayejenga jengo kwenye eneo jipya hakuna kodi. Wekezeni kwenye maeneo maalum hata dhahabu ikiisha mtakuwa na biashara nyingine. Arusha uchumi umekuwa kwa madini.
Tuna Dhahabu halafu tunazungumzia umaskini Geita? Tunakwama wapi? Tuna Masoko 7 katika Masoko 28 Tanzania nzima. Tukae tujadili tutoke na majibu, bado sijaridhika hapa tulipofika kwa kuzalisha kilo 500 kwa mwezi. Nataka tufike kilo 1,000. Vikundi vielimishwe, wawekezaji walete mitambo, taasisi za Serikali zipo, Taasisi za Fedha zipo.
Soko kubwa la Dhahabu liko Dubai na kule hakuna mashimo wala maduara, kwanini na Geita tusiwe na Soko Maalum? Tunataka Geita kuwa kimbilio kwenye biashara Afrika Mashariki kama Dubai.
Uchumi wa madini ni mkubwa sana siyo wa kudharau, tukisimamia vizuri sekta hii tutaongeza mapato ya serikali na kukuza sekta nyingine. Mimi na Timu yangu tunaiangalia Geita kama isiyo na dhahabu kwa kuwa inaweza kuisha muda wowote
Halmashauri zote zina uwezo wa kuongeza mapato kutokana na masoko ya madini.
Naiangalia dhahabu kama kilimo cha mihogo kuna wakati wa kilimo na mavuno, kwenye dhahabu hakuna kupanda ni kuvuna tu na hakuna wadudu waharibifu, tujipange.
Viongozi tuwe na maono ya kipekee ili tulete uchumi wa Viwanda Geita kupitia Madini. Tumefungua hifadhi kule Burigi Chato wadau wa madini mnaweza kufanya biashara kwenye maeneo ya utalii, fursa zipo.
Mtu angeniuliza ni yapi maeneo bora ya kukidhi Viwanda hapa nchini na Geita imo tunaweza kupelekea bidhaa katika nchi za Rwanda, Uganda na nchi nyingine. Wafanyabiashara tuwekeze kwenye uchumi mwingine kupitia madini.
Majadiliano yalenge changamoto mbalimbali kwenye Sekta ya Madini na kupatiwa ufumbuzi.
Kongamano hilo limehudhuriwa na wadau mbalimbali wa madini wakiwemo wachimbaji, wafanyabiashara wa madini, kampuni za madini, Taasisi za Fedha na Taasisi za Serikali.
Mada zinazojadiliwa katika kongamano hilo ni pamoja na, Madini ni Chachu ya kukuza Viwanda kwa maendeleo Jumuishi na endelevu mkoa wa Geita kwa kuzingatia mchango wa wachimbaji; Utafutaji na Uchimbaji wa Madini (Fursa na Changamoto); Mazingira , Usalama na Sekta ya Madini, Ubora na Viwango na Vipimo.
Mada hizo zinatolewa na wataalam mbalimbali kutoka Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST), Chuo Kikuu Huria Tanzania, Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, OSHA, Wakala wa Vipimo na TBS.
TEITI Office Dodoma
Postal Address: S.L.P 361 Kikuyu Ave.
Telephone: +255688386546
Mobile: +255688386546
Email: info@teiti.go.tz
Haki Miliki ©2017 TEITI .Haki zote Zimehifandiwa